Thursday, 3 November 2011

UJENZI WA CHUO KIKUU WILAYANI KARAGWE NA JUHUD FELIX

Zaidi ya shilingi milioni 800  zinatakiwa kukamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha kanisa la Kilutheri Dayosisi ya Karagwe kinachotarajiwa kuanza ujenzi wake Juni mwaka huu.

Hayo yamesemwa jana na mchungaji Daktari Brighton Katabaro ambaye pia ni mratibu wa uanzishwaji wa chuo kikuu Karagwe wakati akisoma taarifa ya azma  na mchakato wa uanzishwaji chuo kikuu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kayanga wilayani hapa.

Daktari Katabaro alisema kuwa ili kukamilisha ujenzi wa chuo kikuu hicho zaidi ya shilingi milioni 800 zinatakiwa ili kusiwepo na kukwama ujenzi utakapoanza  katika kata ya Kihanga  kijiji  cha Kishoju wilayani Karagwe.

Daktari alisema kuwa fedha hizo zitapatikana kutokana na michango mbalimbali ya wananchi ,Taasisi za kiserikali ,na zisizo za kiserikali pamoja na kuchangia kwa njia ya harambee ili kufanikisha azma ya ujenzi wa chuo kikuu.

Alisema kuwa Dayosisi inayo ardhi kubwa na ya kutosha kabisa kwa ujenzi wa chuo kikuu zaidi ya hekta 372 zilizoko katika kijiji cha Kishoju,kuwa dayosisi ya Karagwe inaazimia kuanzisha chuo hicho  chenye mchepuo wa kilimo na stadi za mazingira ili kuchangia kuinua hali ya maisha ya watanzania haswa wanaoishi vijijini wakitegemea kilimo na ufugaji  kama uti wa mgongo wa maisha.

Aidha Daktari Katabaro alisema kuwa chuo kikuu cha Karagwe yaani Karagwe Universty  College(KARUCO) kitasaidia kuchochea matumizi ya zana za kisasa za uzalishaji na hivyo kuongeaza tija na kuboresha mazao mengi ya kilimo yanayozalishwa wilayani hapa.

Kwa upande wake  Askofu Daktari Benson   Bagonza  alisema kuwa chuo hicho  kitatoa fursa nyingi kwa wananchi zinazolenga  kutokomeza umaskini zikiwemo fursa ya elimu,Kiuchumi, kibiashara,kimiundo mbinu,kiafya na kimawasiliano.

Daktari Bagonza alisema kuwa licha ya kilimo na ufugaji  chuo kikuu kinakusudia  kuandaa walimu wenye  shahada  na stashahada  katika sanaa ,sayansi na biashara ili kuongeza idadi  ya walimu  hasa katika  shule za sekondari  wilayani  Karagwe.

Hata  hivyo Daktari  Bagonza alisema dayosisi itaendelea na jitihada za kushirikisha wadau mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi ili kupata fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho kuwa wapo wafadhili wa nje waliokwisha waunga mkono na kuonyesha dalili za kushirikiana na dayosisi katika mchakato huo.


Na
    Juhudi   Felix

No comments:

Post a Comment