Thursday, 3 November 2011

WANANCHI TUKITAKA KIONGOZI BORA ATAKAYE TUFAA AWE NA SIFA HIZI ZIFUATAZO KULIKO KUPEWA POMBE NA PESA ZA MUDA WA KAMPEINI TU.

Ni wazi kuwa nchi yetu kwa sasa iko kwenye vuguvugu la uchaguzi mkuu wa kuwapata madiwani,wabunge, wawakilishi huko Zanzibara  na rais kwa Tanzania Bara na Visiwani.

Na kipindi hiki ndicho watu kadhaa wanajaribu kupita kila kona ya nchi hii kwa nia ya kujitangaza ili muda ukifika waweze kuingia katika kinyanganyiro cha kuwania kuingia kwenye madaraka.

Napenda kutumia fursa hii kufikisha ujumbe kwa Watanzania wenzangu haswa wanaoishi maeneo ya vijijini ambako ndiko kuna walio wengi na hawana sehemu ya kupaza sauti zao hivyo njia pekee ni kuwa makini na watu wanaotaka kuingia madarakani kwa zawadi za muda mfupi yaani muda wa kampeini tu na ukiisha utasikia anaishi Dar es salaam na kipindi cha uchaguzi mwingine ukiwadia utamuona anarudi na kuwa karibu  na wananchi.



Kwa leo ninaomba watanzania tuwape masharti au tuchague watu wenye sifa za kujali na kuheshimu utawala wa kidemokrasia kuanzia ngazi ya kitongoji,kijiji/mtaa ili kuutambua mchango wa maeneo hayo  na kujua vipaombele vya wananchi wa maeneo husika ili kuleta  maendeleo ya kweli kuliko kuja na mipango inayokuwa kwenye vitabu na badala yake inakuwa kama ya kufikirika.

Moja ya mambo ambayo anapaswa kuyafahamu ni pamoja na kuwa serikali inatambua uwepo wa serikali za mitaa/vijiji na huko ndiko watanzania walio wengi wanakoishi hivyo ajue kuna vipaombele vyao.

Hivyo atakeyekuja anataka kutumikia wananchi kama wanavyodai wakati wakijinadi ni wazi tunataka awe anafahamu kuwa mwananchi anao wajibu na majukumu yake ya kuhakikisha  kuwa kiongozi atakaye mchagua awe anatimiza wajibu wake ipasavyo katika viwango vinavyokubalika kisheria kwenye eneo husika kama ni mtaa, kitongoji, kijiji  wilaya na Taifa kwa ujumla.




Pia wananchi wana jukumu la kudai na kupigania haki zao na za wananchi wengine  kutoa malalamiko  na kuuliza maswali juu ya mambo  mbalimbali yanayoendelea kijijini au kwenye  mtaa na sehemu nyingine  kupitia vyombo  mbalimbali vya kijamii na kiserikali.Na kila mwananchi anao wajibu wa kupinga na kukataa kila aina ya  uovu  katika jamii  ikiwemo rushwa, uonevu,wizi ubadilifu wa mali za umma nay a watu binafsi.

Kiongozi atakaye tufaa zaidi ni huyu atakayekuwa tayari kutekeleza mambo haya awe anajua ushiriki wa wananchi katika suala zima la kujiletea maendeleo,ushirikishwaji wa wananchi katika kutekereza sera mbalimbali za serikali,uwazi na wajibikaji  katika shughuli za maendeleo, kuwa na uwazi katika taarifa za mapato na matumizi,kudhibiti  matumizi ya rasilimali katika maeneo au jimbo analotaka kugombea.

Vilevile mtu anayetaka kugombea iwe nafasi ya udiwani au ubunge inabidi atambue kuwa wananchi wanawajibu wa  kulinda mali,rasilimali za umma na kupambana na kila aina ya uovu ukiwemo ubadilifu,wizi ,rushwa na mengineyo ambayo hayastahili katika jamii. 

Kiongozi atakayekuwa tayari kujenga na kuimarisha mshikamano uliopo katika jamii,kushiriki kusimamia miradi ya wananchi,kuheshimu wananchi na wapigakura wake ili kuleta dhana nzima ya kiongozi bora.

Aidha mtu anayetaka kupata nafasi anayoiwania ni lazima ajue maana ya umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi kutofanya hivyo kunasababisha miradi mingi inayoibuliwa kutokuwa na ufanisi kwani wananchi wakishirikishwa wataweza kuibua miradi mingi ya maendeleo na hiyo itafanywa na kiongozi anayejua wajibu wake.

Wananchi kama tukitaka kumjua kiongozi atakayetufaa ni kuwa baada ya kuelezwa mambo haya ata hiari kuyatekeleza na kama siyo hivyo wananchi tusiwe tayari kumchagua lakini zipo dalili na sifa nyingi ila nimeweza kuainisha hizi ili  tuwe makini na watu wanaotoa hongo ya pombe,nguo kwa lengo la kujipatia nafasi ambazo wanazihitaji hii ni hatari kwani kufanya hivyo ni kuuza haki zetu za msingi.

Hata Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anasisitiza hili kuwa tuwe makini na watu wanaotumia utajiri wao wa pesa kuwanunua wananchi ili kujipatia madaraka nah ii anaipigia kelele mara kwa mara hivyo ni wajibu wetu wa kuchambua na kutafakari kwa mapana.

Watanzania wenzangu ni ukweli usiopingika kuwa hali ya tete ambayo ilijitokeza ya ubadilifu wa mali za umma kwa kipindi kilichopita iko mikononi mwetu sasa kuchambua na kuchuja kuangalia ni mtu gani wakutufaa kutuongoza kwa kufuata misingi iliyowekwa ya uadilifu uaminifu na asiyetaka kujilimbikizia mali mwenye kujali maslahi ya wapigakura na wananchi wake na Taifa kwa ujumla.

Pia watanzania wakati wa kufanya kile Rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete cha kutaka kutungwa sheria ya kutenganisha siasa na biashara imo mikononi mwetu kuonyesha njia kwani sisi ndio wapiga kura inabidi kuchagua kwa kuangalia vigezo vya ushirikishwaji,uwajibikaji hapo tujiulize mtu kama ni mfanya biashara atakuwa na muda wa kukaa na nyinyi saa ngapi kupanga mambo ya miradi ya maendeleo au atajili maslahi yake ili asiweze kupata hasara kwenye shughuli zake.

Kuna kundi la wagombea wengine wanakuja kwa staili ya kuwa nimeombwa na wazee ili niweze kugombea nafasi husika ili niweze kuwaletea waqnanchi wa kata fulani au jimbo fulani  wazee tu ndio wenye maamuzi ya maendeleo tu au ni wananchi kwa pamoja na pia tujiulize hao wazee wanakaa kikao wapi na wanatoa tamko wapi la kuwataka kugombea nafasi hizi kama sikutumia mgomgo huo wa wazee kujitangaza?



Watanzania tutambue kuwa matatizo ya utovu wa Uadilifu umewakumba viongozi wengi  wa kuchaguliwa na wa kuteuliwa kiasi cha kuzidisha uzito wa matatizo yanayoelezwa kwenye sehemu mbalimbali utovu huo umezaa rushwa,ubadilifu,utendaji kazi wa mazoea.

Wananchi wenzangu kiongozi atakayetufaa ni yule atakaye shirikiana nasi katika harakati za kujikwamua katika hali duni za maisha  na umaskini uliokithiri,ukosefu wa huduma bora kutokana na udhaifu wa hali ya uchumi na kukosa kiongozi imara,ambao umefanya vita dhidi  ya umaskini ,maradhi  na ujinga iwe ngumu zaidi.

Kiongozi ambaye atajali na kusaidia kukamilika miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo huimbuliwa na wananchi kupitia mpango wa fursa na vikwazo yaani O&OD ili iweze kukamilika na kuleta ufanisi. Atakayekuwa tayari kusimamia sera za serikali ili kuimarisha mfumo wa uwajibikaji kwa wananchi ili taifa liwe na umoja.

Mtu ambaye anafuata sera ya utawala bora kwa kutumia mfumo wa upelekaji wa madaraka na majukumu  na rasilimali kwa wananchi (Decentralization by Devolution)yaani ugaduzi ulioigwa katika nchi ya Bangaladeshi na ambao unatumika sasa kwenye serikali za mitaa ambako ndio kuna watanzania wengi.

Ni sifa nyingi ambazo tunataka kiongozi tunayemuhitaji kututumikia na si bora kiongozi hivyo tuwe makini katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu hapo Oktoba mwaka huu na ndio maana kupitia safu mbalimbali tunajaribu kutoa kidogo tulichonacho ili tuweze kuwa na wawakilishi wazuri wasio jail maslahi yao binafsi bali ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ninapatikana kwa mawasiliano na 756 601054 au felixjuhud@yahoo.com

No comments:

Post a Comment